Sababu za wasichana kuongoza kwa maambukizi ya VVU

NA ELBOGAST MYALUKO
Baada ya Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) kutoa takwimu hivi karibuni ambazo zinazoonesha kundi linalopata maambukizi mapya ya VVU, ni vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24, huku asilimia kubwa wakiwa ni wasichana leo imetaja sababu zinazopelekea hilo.


  • TAZAMA VIDEO HII KISHA SUBSCRIBE YOUTUBE

 Akiongea kwenye Kipindi cha Mjadala kinachoruka kupitia East Africa Television, Mkurugenzi wa Uraghibishi na Habari wa TACAIDS Bw. Jumanne Issango, ametaja maamuzi kwenye mahusiano ndio sababu kubwa ya wasichana wengi kupata maambukizi kuliko wavulana.

Ameeleza kuwa kutokana na mila zetu mara nyingi mwanamke hana maamuzi juu ya mwili wake hususani kwenye mahusiano ambapo hata matumizi ya kinga hutegemea mwanaume anasemaje na si suala la makubaliano baina yao.

''Kundi hili linaathirika sana kwasababu huwa wanategemea maamuzi ya watu wengine kuanzia kuolewa na hata kwenye suala la maisha ni wachache wenye uwezo wa kujihudumia lakini wengi wao hujikuta kwenye vishawishi vya wanaume ili wapate mahitaji yao'', amesema.

Ameongeza kuwa suala la kurubuniwa mara nyingi kijana wa kiume halimhusu sana kwani yeye ndiye anayeweza kumrubuni msichana na ni mara chache kwa msichana kumrubuni mvulana.

Takwimu zilizotolewa hivi karibuni na TACAIDS zinaonesha kuwa katika asilimia 100 za vijana wanaopata maambukizi mapya kati yao asilimia 80 ni wasichana na asilimia 20 pekee ndio wavulana, hivyo kufanya katika kila vijana 10 wenye maambukizi mapya ya VVU nane ni wasichana na wawili ni wavulana.

Comments