Watu Waliokutwa na tausi wa Ikulu wahukumiwa kulipa Milioni 6


Watu watatu wanaodaiwa kukutwa na ndege aina ya tausi wa Ikulu wamehukumiwa kulipa fidia zaidi ya Sh6.8 milioni baada ya kukutwa na hatia katika kesi ya uhujumu uchumi kwa kujihusisha na nyara za Serikali bila kibali.

Kadhalika mahakama hiyo imetaifishwa ndege hao kuwa mali ya serikali. Pia imewaachia huru kwa masharti ya kutokutenda kosa ndani ya miezi sita.

Hukumu hiyo ilisomwa jana na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Salumu Ally, baada ya washtakiwa kumwandikia Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) barua ya kukiri makosa yao.

“Mahakama hii inawaamuru washtakiwa kulipa fidia ya Sh. 6,890,000, ndege hao wanataifishwa kuwa mali ya serikali na inawaachia huru kwa masharti kwamba wasitende kosa la jinai ndani ya miezi sita,” alisema Hakimu Ally wakati akisoma hukumu hiyo.

Awali, washtakiwa walidaiwa kujihusisha na genge la uhalifu, kukutwa na nyara za serikali ikiwamo ndege aina ya tausi watatu wa Ikulu ya Tanzania.

Washtakiwa hao ni David Graha, Mohammed Hatibu na Mohammed Mahamoud, wote wakazi wa jijini Dar es Salaam.

Washtakiwa hao walisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Vick Mwaikambo.

Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai kuwa shtaka la kwanza, kati ya Juni Mosi, 2015 na Oktoba 14, mwaka huu waliratibu mipango ya uhalifu kwa kujihusisha na biashara ya ndege hao wenye thamani ya Dola za Marekani 1,500 (sawa na Sh. 3,444,150).

Nchimbi alidai katika shtaka la pili, washtakiwa walikutwa na ndege watatu aina ya tausi wenye thamani hiyo ya fedha.

Wankyo alidai katika shtaka la tatu, Oktoba 14, mwaka huu eneo la Mikocheni, mshtakiwa wa tatu Mahamoud alikutwa na tausi hao.

Comments