Mwanangu..Utakapojenga Nyumba Yako Usisahau Haya


Na. Robert Heriel.


Mwanangu huu ni muendelezo wa barua zangu kwako. Niwie radhi ikiwa nimeandika kirefu mpaka nikakuchosha kusoma. Sio dhamira yangu kukuchosha bali natazamia kuwa kupitia maandiko haya utakuwa mtu bora kwa zama zako.

Nawe utakapo kuwa mtu mzima. Mungu akakubariki na kukupa utajiri. Nawe ukajenga nyumba yako. Basi utamshukuru Mungu wa Baba yako. Naye utamsifu siku zote za maisha yako.


Nawe utajenga nyumba kubwa yenye kukutosha wewe na wanao, na watumishi, na wageni. na mifugo yako usisahau.

Utajenga nyumba yenye vyumba kulingana na watoto utakao wazaa. Kama ni wanne basi vyumba vinne. Lakini kama hali ya uchumi haitakuruhusu basi ujenge nyumba yenye chumba chako na mkeo. Pia vyumba vya wana wa kike na wana wa kiume.

Vyumba vya wanawa kiume viwe karibu na mlango wa kutokea mlango wa nje. Na vyumba vya wana wa kike viwe karibu na chumba chako na mkeo.

Ikiwa Mungu atakubariki basi jenga nyumba kubwa yenye vyumba kulingana na idadi ya watoto wako. Zungushia Uzio iwe ni matofali au uzio wowote kulingana na teknolojia ya wakati wako.

Uzio uwe na urefu wa futi saba kwenda juu. Ili mambo ya nyumba yako yawe ya nyumba yako kikamilifu. Nawe utakapojenga uzio katika nyumba yako utajiepusha na mikosi na laana. Ili kwamba mtu asije akauawa huko mitaani akaja kufia katika eneo la uwanja wako. Usije ukaitia laana na mikosi nyumba yako. Ndio maana nikakugiza ujenge uzio kuzunguka nyumba yako. Kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Torati naam ndicho kile kitabu chema sana.

Ndani ya uzio wa nyumba yako utajenga nyumba ndogo za wageni na watakao kuja kukutembelea. Halikadhalika na vyumba vya watumishi utakao waajiri katika nyumba yako.

Vyumba vya nje watalala wageni. Wala usimruhusu mgeni yoyote alale na watoto wako uliowazaa. Tena usiwe na imani na mtu yeyote hata kama ni ndugu yako. Kamwe usimlaze mtu yeyote na wanao wa kuwazaa. Hivyo ndivyo utakavyoepa na kukimbia madhara katika nyumba yako.

Nawe utajikinga na athari za wazi na za siri ndani ya nyumba yako.

Nakuambia haya kwa kuwa zama zenu ni zama mbaya sana. Watu wameharibika akili na roho. Usije ingiza desturi mpya ndani ya nyumba yako. Hata watoto wako wasijewakaharibiwa mwili na roho kwa matendo ya uasherati.

Naye watoto wenu wafikishapo umri wa miaka miwili watengeni nanyi. Msilale pamoja na watoto wenu wenye umri kuanzia miaka miwili. Watengeni wajitegemee wenyewe usiku walalapo.

Nawe utapanda miti aina aina ya matunda ndani ya uzio wa nyumba yako. Migomba ya ndizi, Mipapai, miembe, michungwa, Miparachichi na miwa kwa kadiri utakavyoona. Tena usisahau kulima hata bustani ya mbogamboga.

Utapanda miti ya matunda ili upate chakula kupitia miti hiyo. Hata siku ukikosa pesa ya chakula usiilaze familia yako njaa. Utamwambia mkeo; Mke wangu nikupendaye. Tazama leo hatuna hela ya chakula. Nenda huko bustanini unaweza pata hata mkungu wa ndizi au hata matunda yatuvushe siku ya leo.

Tena ndege watakutembelea kila siku nyumbani kwako. Hata wageni wajapo hutakosa chochote cha kuwapa mkononi siku wakirudi makwao. Kamwe mgeni ajapo kwako asirudi mikono mitupu.

Nawe utajipatia dawa za kienyeji katika miti hiyo na katika bustani uipandayo. Tena utapata hewa safi na vivuli kwa afya yako.

Na kama hutafanya niliyokuambia ndipo utakapo jiona masikini. Tena utakuwa mchoyo. Wageni watakutembelea nawe utakosa kitu cha kuwapa mkononi.

Tena magonjwa yatakuandama kila mara. Magonjwa ya kupumua, Ya mfumo wa damu, magonjwa ya ngozi, Na magonjwa ya utumbo yote yatakuandama. Hata mfumo wa mkojo hautabaki salama.

Nawe utafuga Wanyama wa nyumbani kama vile kuku, njiwa, paka, Mbwa, ng'ombe, mbuzi na wengineo kwa kadiri ya wale uwapendao. Hao uwapende sana. Tena uwaheshimu na kuwathamini kwa kuwa ndio watakao kusaidia kwa ulinzi na chakula. Tena utapata mbolea itakayokusaidia katika kilimo.

Usijenge katikati ya mji bali jenga pembezoni mwa mji yaani nje ya mji. Ili upate eneo kubwa la kufanyia mambo yako.

Kwa maana itakusaidia nini kukaa katikati ya mji ilhali huna uwezo wa kufadhili wageni. Huna uwezo wa kulisha familia yako. Ni bora uishi nje ya mji lakini unauwezo wa kujimudu na kufadhili wageni.

Nawe katika nyumba yako usiweke picha ya mtu yeyote isipokuwa ya wanafamilia. Tena uweke maandiko ya hekima katika miimo ya malango yako na katika kuta zako.

Utajenga Vyoo vya ndani katika nyumba yako. Nawe usishiriki choo kimoja na watoto Bali choo chako na Mke wako kitakuwa ndani kabisa. Ili utakapokuwa ukienda kujihifadhi watoto wasikuone. Halikadhalika na Mke wako wasimuone. Kwa maana wewe ni Baba wa familia hupaswi kuonekana kwa mambo kama hayo.

Utajenga vyoo viwili vya nje vya wageni na watumishi wa nyumba yako. Choo kimoja cha wanawake na kingine cha wanaume. Ili hata kutakapotokea sherehe au msiba katika nyumba yako watu wapate pakujihifadhi.

Utaacha nje eneo kubwa la kupumzikia wageni. Huo utakuwa ukumbi wa nje. Utaupanda nyasi fupi ziitwazo ukoka. Eneo hilo litakuwa rasmi kwa mapumziko na mikusanyiko ya watu wakati wa matukio ya sherehe na maombolezo.

Nawe usijenge Nyumba ya Ghorofa kwenda Juu. Kwa maana utakapokuwa mzee hutaishi katika ghorofa hizo kutokana na miguu kuchoka kwa uzee. Lakini kama Utakuwa na Nyumba nyingi haidhuru unaweza kujenga. Kama huna ni bora hizo hela ulizojengea ghorofa ujenge nyumba zingine zisizo na ghorofa. Kwa kuwa kujenga ghorofa ni gharama sana.

Usipande miti isiyovutia ndege wa angani. Tena miti isiyokaliwa na ndege wa angani usiipande katika nyumba yako.

Nawe usiache taa zikawaka mchana. kwa maana huo ni ubadhirifu wa mali. Tena uwe makini katika kutumia mali za nyumba yako. Usiache Redio na Luninga vikiongea kwa pamoja. Au kimoja wapo kikifanya kazi(kuongea au kuimba) wakati hakuna msikilizaji au mtazamaji. Huo ni ubadhirifu wa mali.

Utafunga mlango kila uwapo ndani ya nyumba. Iwe ni usiku au mchana. Funga na Kufuli kabisa. Usiache mlango wazi ukiwa ndani au nje. Hii itakusaidia kupunguza hatari ya kuibiwa.

Usiache funguo mlangoni. Wala usitembee na funguo ya nyumba yako barabarani. Tafuta sehemu ya siri uifiche. Hakikisha ni sehemu iliyojificha haswa. Tena Funguo utakayoificha iwe ni moja tuu ya kufungulia mlango wa Nje tuu. Hizo funguo zingine zibaki ndani ya nyumba. Mahali palipojificha ambapo si rahisi kuonekana.

Nawe kabla hujalala usiku hakikisha umefunga bomba za maji, hakikisha umefunga milango yote, Hakikisha umezima taa za ndani lakini taa za nje usizizime. Ili nje kuwa na mwanga wezi wasijekupata sehemu za kujificha. Na kama utasikia usiku Maji ya bomba yanamwagika iwe ni kwenye tanki kubwa au maji ya namna yoyote ile. Kamwe usitoke nje. Ndio maana nikakuambia hakikisha uwe umefunga bomba zote.

Kwa maana wezi na majambazi huweza kufungulia bomba la maji nje ili utoke nje wakudhuru.

Nawe usiku utafungulia Mbwa. Kama unafuga mbwa wa wawili itapendeza. Mbwa mmoja utamfunga mnyororo lakini mwingine utamuachia(Kwa wakati wa usiku). Mchana wote utawafunga minyororo au bandani.
Mbwa mmoja atakuwa mlinzi na kama atapewa sumu basi atabaki mbwa aliyefungwa minyororo akibweka mpaka utakapo amka.

Usitoke kupambana na wezi au majambazi kama hujawaona. Kaa ndani ukiwasiliana na Vyombo vya ulinzi mpaka vitakapokuwa vimekuja. Usiwashe taa za ndani ukiwa katika hatari. Tena ikiwezekana zima mpaka taa za nje kwa dakika tano kisha ziwashe tena kwa dakika moja. Fanya hivyo hivyo. Kuwa na tahadhari siku zote.

Usiweke Sakafu ya kuteleza hasa maeneo ya jikoni na bafuni au Chooni. Tena pasiwe na mti karibu na nyumba yako au dirisha lako au dirisha la watoto wako.

Nawe utaamka alfajiri na mapema kila siku kuomba na kusali. Wewe na Mke wako. Wewe na watoto wako. Wewe na watumishi wako na kila aliyeko katika nyumba yako atasali na kuomba alfajiri kwa Mungu wa Baba yako. Utawafundisha yale niliyokufundisha.

Na itakapofika usiku utaomba na kusali. Wewe na Mke wako. Wewe na watoto wako. Wewe na watumishi wako na kila aliyemo katika nyumba yako. Utamuomba Mungu wa Baba yako. Utawafundisha watoto wako yale niliyokufundisha.

Nawe usiingize mwanamke mwingine ndani ya nyumba yako. Tena asitokee mtoto wako au mtumishi wako au yeyote aliyeko katika nyumba yako akafanya uzinzi katika nyumba yako.

Kama itatokea ni mwanao wa kumzaa akafanya hayo. Basi mfukuze usimuonee huruma. Na kama Mke wako atafanya hila na kumficha mzinzi au mchawi ndani ya nyumba yako. Siku utakayobaini mfukuze wala usimuonee huruma. Kwa maana amekuficha uovu wa mtoto wako. Hivyo alishiriki kumpoteza mtoto wako uliyepewa na Mungu wa Baba yako. Mfukuze usimuonee huruma.

Nawe usipokee mgeni atakayebisha nyumbani kwako zaidi ya saa nne za usiku bila taarifa. Huyo usimpokee kwa maana hakutoa taarifa naye amekuja usiku bila taarifa.

Nawe usiwe na dini mbili ndani ya nyumba moja. Yaani wewe na Mkeo muwe na dini moja. Kama atakuwepo mtu wa dini nyingine katika moja ya watumishi wako au wageni wako au mtu yeyote akaaye katika nyumba yako. Basi hakikisha dini hiyo umeithibitisha.

Comments